Jeremiah 15

Adhabu Isiyoepukika

1 aKisha Bwana akaniambia: “Hata kama Musa na Samweli wangesimama mbele zangu, moyo wangu usingewaelekea watu hawa. Waondoe mbele za macho yangu! Waache waende! 2 bNao kama wakikuuliza, ‘Twende wapi?’ Waambie, ‘Hili ndilo Bwana asemalo: “ ‘Wale waliowekwa kwa ajili ya kufa, wakafe;
waliowekwa kwa ajili ya upanga, kwa upanga;
waliowekwa kwa ajili ya njaa, kwa njaa:
waliowekwa kwa ajili ya kutekwa, watekwe.’ ”

3 c Bwana asema, “Nitatuma aina nne za waharabu dhidi yao: nazo ni upanga ili kuua na mbwa ili wakokote mbali, ndege wa angani na wanyama wa nchi ili kula na kuangamiza. 4 dNitawafanya wawe machukizo kwa falme zote za dunia kwa sababu ya kile alichofanya Manase mwana wa Hezekia mfalme wa Yuda huko Yerusalemu.
5 e“Ni nani atakayekuhurumia, ee Yerusalemu?
Ni nani atakayeomboleza kwa ajili yako?
Ni nani atakayesimama ili kuuliza
kuhusu hali yako?

6 fUmenikataa mimi,” asema Bwana.
“Unazidi kukengeuka.
Hivyo nitanyoosha mkono wangu juu yako na kukuangamiza,
siwezi kuendelea kukuonea huruma.

7 gNitawapepeta kwa uma wa kupepetea
kwenye malango ya miji katika nchi.
Nitaleta msiba na maangamizi juu ya watu wangu,
kwa maana hawajabadili njia zao.

8 hNitawafanya wajane wao kuwa wengi
kuliko mchanga wa bahari.
Wakati wa adhuhuri nitamleta mharabu
dhidi ya mama wa vijana wao waume;
kwa ghafula nitaleta juu yao
maumivu makuu na hofu kuu.

9 iMama mwenye watoto saba atazimia
na kupumua pumzi yake ya mwisho.
Jua lake litatua kungali bado mchana,
atatahayarika na kufedheheka.
Wale wote waliobaki nitawaua kwa upanga
mbele ya adui zao,”
asema Bwana.


10 jOle wangu, mama yangu, kwamba ulinizaa,
mtu ambaye ulimwengu wote
unashindana na kugombana naye!
Sikukopa wala sikukopesha,
lakini kila mmoja ananilaani.

11 k Bwana akasema, “Hakika nitakuokoa kwa kusudi jema,
hakika nitawafanya adui zako wakuombe msaada
nyakati za maafa na nyakati za dhiki.


12 l“Je, mtu aweza kuvunja chuma,
chuma kitokacho kaskazini, au shaba?

13 mUtajiri wako na hazina zako nitavitoa kuwa nyara,
bila gharama,
kwa sababu ya dhambi zako zote
katika nchi yako yote.

14 nNitakufanya uwe mtumwa wa adui zako
katika nchi usiyoijua,
kwa kuwa katika hasira yangu moto umewashwa
utakaowaka juu yako daima.”


15 oWewe unafahamu, Ee Bwana,
unikumbuke na unitunze mimi.
Lipiza kisasi juu ya watesi wangu.
Kwa uvumilivu wako usiniondolee mbali;
kumbuka jinsi ninavyoshutumiwa.

16 pManeno yako yalipokuja, niliyala;
yakawa shangwe yangu
na furaha ya moyo wangu,
kwa kuwa nimeitwa kwa jina lako,
Ee Bwana Mungu Mwenye Nguvu Zote.

17 qKamwe sikuketi katika kundi la wafanyao sherehe,
wala kamwe sikujifurahisha pamoja nao;
niliketi peke yangu kwa sababu mkono wako ulikuwa juu yangu,
na wewe ulikuwa umenijaza hasira.

18 rKwa nini maumivu yangu hayakomi,
na jeraha langu ni la kuhuzunisha,
wala haliponyeki?
Je, utakuwa kwangu kama kijito cha udanganyifu,
kama chemchemi iliyokauka?

19 sKwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana: “Kama ukitubu, nitakurejeza
ili uweze kunitumikia;
kama ukinena maneno yenye maana,
wala si ya upuzi,
utakuwa mnenaji wangu.
Watu hawa ndio watakaokugeukia,
wala si wewe utakayewageukia wao.

20 tNitakufanya wewe uwe ukuta kwa watu hawa,
ngome ya ukuta wa shaba;
watapigana nawe
lakini hawatakushinda,
kwa maana mimi niko pamoja nawe
kukuponya na kukuokoa,”
asema Bwana.

21 u“Nitakuokoa kutoka mikono ya waovu,
na kukukomboa kutoka makucha ya watu wakatili.”
Copyright information for SwhKC